Waziri wa Katiba na Sheria, Dk.Asha-Rose Migiro.
Kwa hivyo basi, nitumie fursa hii hapa kuzitofautisha dhana hizi
mbili yaani ubia na uwakala. Ufafanuzi unaotolewa hapa unaweza kutokidhi
kiu ya mwanazuoni wa lugha, kwa vile nayafafanua maneno haya kwa vile
yanavyoeleweka kisheria.
Kisheria mambo yote mawili, yaani ubia na mkataba, ni mahusiano
yanayoangukia katika sheria za mikataba ingawa wasomi mahiri
walioyachimba mambo haya kwa kina zaidi (kama alivyo Mwingereza Lindley,
kinara wa sheria za Ubia) wameweza kuvifanya vipengele hivi kuanza
kuonekana kama vinavyojitegemea kutokana na utata utokeao ndani ya mambo
haya ya ubia na uwakala. Kwa hivyo basi, iwapo tunafuata utaratibu huu
basi, Sheria ya Ubia huitwa Partnership Law (kimombo) wakati ile ya
Uwakala inaitwa Agency Law.
Kwa hapa Tanzania, Sheria ya Mikataba ambayo ni Sura ya 345 ya Sheria za nchi inazifafanua dhana hizi kirefu.
Sheria hii ya mwaka 2002 haina tofauti sana na ile ya awali ya
mwaka 1961, isipokuwa imeyaweka bayana zaidi masuala yaliyokuwa yakileta
utata ndani ya sheria hii, kati ya mwaka 1961 hadi 2002 sheria zetu
nyingi zilivyohakikiwa tena, ambapo sasa hata zile tafsiri za sheria ya
awali, kama zilivyotolewa na Mahakama Kuu na ile ya Rufaa pamoja
zimezingatiwa kwa kuingizwa au kukataliwa.
Uwakala (Agency) umefafanuliwa katika Sehemu 10 ya Sheria hii,
wakati ambapo Ubia (partnership) umewekewa misingi yake na kufafanuliwa
kisheria katika sehemu ya 11 ya Sheria hiyo hiyo.
Kwa ujumla wake, ukivisoma vifungu vyote 54 (kuanzia kifungu cha
134-189) ambavyo vinajikita katika kufafanua maana, haki na wajibu wa
wahusika katika masuala ya Uwakala kisha ukavilinganisha na vifungu
vyote 36 (yaani kuanzia kifungu cha 190-226) huku ukizingatia misingi na
sheria nyinginezo, basi mambo haya yafuatayo yanaweza kubainishwa
kuhusu kushabihiana (kufanana) au kutofautiana kwa ubia na uwakala:
(1)Ubia na Uwakala, vyote viwili vinaangukia katika sheria za
mikataba. Kwa maana hii basi, unapohitajika ufafanuzi Sheria za mikataba
zinatumika zaidi.
(2)Ubia (partnership) unafanana na uwakala (agency) kwa kuwepo
zaidi ya mtu mmoja katika kufanikisha hicho kinachofanyika ama kukusudia
kufanyika. Bila watu wawili ama zaidi hakuna ubia na bila watu wawili
au zaidi hakuna uwakala pia. Huwezi kufanya ubia peke yako na huwezi
kufanya uwakala peke yako. Kwa ufasaha zaidi ni kuwa mtu mmoja pekee
anaweza kufanya biashara anamiliki pekee lakini atahitaji mtu au wengine
zaidi kufanya ubia au uwakala uwepo.
(3)Tofauti kubwa ya ubia na uwakala ni kuwa katika ubia wahusika
wanakubaliana kufanya jambo kwa pamoja, wakizingatia mchango wa pamoja,
kugawana faida, hasara na kadhalika lakini kwenye uwakala, kitu hiki
hakipo kwa sababu muuza vocha anayeuza vocha za kampuni fulani ya simu
(vodacom, tigo, Airtel, Zantel, Ttcl na kadhalika) yeye ataendelea
kidunduliza faida hata kama hukuwa na ubia na kampuni ambayo anauza
vocha zake imeingia hasara kubwa kama kampuni.
Yeye hakimgusi kwa sababu si mmliki (mwanahisa) na wala hana kitu
cha pamoja kinachowaunganisha kama daraja (kwa maana ya ubia sasa) na
kampuni hiyo.Hasara wangegawana ubia kama upo.
Mfano wa hapa ni kampuni ya magari ya TOYOTA iingie ubia wa kutumia matairi ya MICHELIN na yakishauzwa wagawane faida.
Iwapo inatokea magari ambayo yangeuzwa yanapata hasara, wote wawili
hawa watapata hasara na iwapo watauza na kupata faida basi wawili
wanafaika na faida hiyo kama wabia.
(4)Katika ubia wahusika wanaweza kuwa na hadhi na nguvu
zinazofanana au kukaribiana na pengine wajibu, haki na maslahi
yanayolingana au kutofautiana kidogo (japo mara chache yakawa na tofauti
kubwa pia) lakini katika uwakala kuna mkubwa na mdogo.
Katika uwakala mkubwa mara nyingi ndiyo hupanga nini kifanywe na
yule anayetoa huduma kama kuuza bidhaa au kutoka huduma kwa niaba yake.
Mara kwa mara huyu mkubwa (Principal) hupanga nini kifanyike na hutoa
sharti ambalo mdogo huwa na nafasi finyu ya kukikataa anachoelekezwa.
Mfano ni mawakala wa LUKU za TANESCO au wauza vocha ama huduma za
kifedha za makampuni ya simu kama M-PESA. Hawa hutekeleza kile ambacho
mkubwa anawaagiza na si rahisi wakala anayeuza kadi za simu kutaka
apangiwe au auze bidhaa bei tofauti na iliyopangwa juu.
Baada ya kuliona hili tusifikiri sasa kuwa, wakala hana haki.
Wakala ana haki kama ambavyo alivyo na wajibu kwa mkubwa wake. Hivyo
hivyo, mkubwa (Principal) ana haki zake kisheria kama alivyo na wajibu.
Sheria ya Mikataba (Sura ya 345) inaelezea wajibu alionao kwa
wakala wake. Mathalani, kifungu cha 174 kinampa haki wakala kufidiwa
katika jambo ambalo limemfanya aingie hasara iwapo jambo hilo alilifanya
kihalali na kwa mujibu wa sheria.
Iwapo, sheria inaelekeza wakala wa kutoa mizigo bandarini afanye
mambo na akayatekeleza kama sheria na utaratibu unavyoagiza na akaingia
hasara. Basi aweza kulipwa fidia kama ambavyo wakala wa kutoa fedha
kibenki anatekeleza sheria ya kutoa fedha kwa niaba ya taasisi fulani na
kukatokea akaingia hasara.
Kifungu cha 175 kinamlinda pia iwapo anaingia, lakini akafanya
jambo fulani likamfanya aingie hasara kama atathibitisha kulifanya kwa
nia njema.
Masuala haya hutegemea ushahidi na kila kesi ni tofauti na nyingine ni vema kupata msaada wa mwanasheria kwa uhakika.
*Denis Maringo ni mwanasheria aliyeko Dar es Salaam. Mawasiliano: dnmaringo@gmail.com (barua-pepe) na 0719270067 (simu).
CHANZO:
NIPASHE